TUTUMIE HABARI NA PICHA MDAU!!

Monday, January 30, 2012

Wezi wa mifugo waua watu 40 Sudan Kusini

Maafisa wa serikali katika Sudan Kusini wanasema watu wasiopungua 40 wameuwawa na kundi la watu wenye silaha waliokwenda kuiba mifugo.

Baadhi ya taarifa zinasema idadi ya watu waliouwawa ni zaidi ya 100 kwenye uvamizi, huo uliotokea kwenye kambi moja katika jimbo la Warrap.

Waziri wa mambo ya ndani wa Sudan Kusini ameilaumu serikali ya Sudan kwa kuwapa silaha washambuliaji hao, ambao ni kundi la wapiganaji kutoka jimbo jirani la Unity.

Mvutano umeendelea kuwepo tangu Sudan Kusini ilipojitenga kutoka Sudan mwezi Julai, kufuatia vita vilivyochukua miaka mingi.

Afisa ammoja katika jimbo la Warrap ameambia gazeti la Sudan Tribune linaloandikiwa mjini Paris kwamba vijiji vinavyokaliwa na watu wa jamii ya Luac Jang katika wilaya ya Tong mashariki walishambuliwa Jumamosi alfajiri.

Spika wa bunge Madot Dut Deng amesema ameambiwa na maafisa kwamba zaidi ya watu 76 wameuwawa, na wengine hajulikani walipo.

Afisa mwingine katika jimbo hilo aliambia gazeti hilo watu katika eneo lililoshambuliwa wanasema waliouwawa ni zaidi ya 100.

Waziri wa mambo ya ndani Alison Manani Magaya amesema mashambulizi hayo yaliendeshwa na kundi la wapiganaji kutoka jimbo jirani la Unity.

"kundi hili lilipewa silaha na serikali ya Khartoum," aliambia gazeti la AFP, lakini hakutaja ni kundi gani.

Sudan Kusini ilipata Uhuru tarehe 9 Julai mwaka 2011 kufuatia vita vya wenyewe kwa wenyewe na Sudan.

Tatizo lililochangia mzozo hadi sasa ni kwamba silaha nyingi zimezagaa.

Kwa habari zaidi endelea hapa: http://www.bbc.co.uk/swahili/habari/2012/01/120130_ssudan_attacks.shtml

0 maoni: