TUTUMIE HABARI NA PICHA MDAU!!

Thursday, March 1, 2012

Padri apongeza tamasha la Pasaka, linatarajiwa kufanyika aprili 8, uwanja wa Taifa

Na Mwandishi Wetu
WADAU nchini wametakiwa kuiunga mkono Kampuni ya Msama Promotions kwa kuandaa matamasha ya Pasaka, yenye lengo la kusaidia matatizo mbalimbali katika jamii. Kauli hiyo ilitolewa jana na Padri wa Kanisa Katoliki Jimbo jipya la Ifakara, Deogratius Kisweka alipozungumza na Jambo Leo kwa njia ya simu. Padri Kisweka alisema kitendo kinachofanywa na Kampuni ya Msama Promotions chini ya Mwenyekiti wake, Alex Msama ni cha kupongezwa. Alisema kila mtu Mungu amempa kipawa chake, hivyo kitendo cha Msama kuandaa matamasha ya injili na kusaidia wajane wasiojiweza, yatima pamoja na kutoa baiskeli kwa walemavu ni jambo la kumshukuru Mungu. "Ni watu wachache ambao wanaweza kufanya kama kinachofanywa na Msama, naamini kila mtu mwenye mapenzi mema anastahili kuunga mkono kwa kuhudhuria tamasha hilo," alisema Kisweka. Pamoja na hilo, Padri huyo aliiomba Kamati ya Maandalizi ya tamasha hilo kutanua wigo kwa kulipeleka katika kila mikoa ili kutoa nafasi kwa wengine kuchangia. Tamasha hilo linatarajiwa kurindima Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, Aprili 8 mwaka huu na pia litafanyika kwenye Uwanja wa Jamhuri mjini Dodoma Aprili 9 mwaka huu. Tayari kundi la muziki wa Injili la Glorious Celebration Spirit of Praise 'Gospel Live' linalotamba na albamu ya Niguse, limethibitisha kushiriki tamasha la Pasaka. Msama alisema mbali na Glorious, waimbaji wengine waliothibitisha kushiriki mpaka sasa ni Upendo Kilahiro, Upendo Nkone na Atosha Kissava kutoka Mkoa wa Iringa. Mbali na Tanzania, pia kutakuwa na waimbiaji kutoka Kenya, Uganda, Zambia, Afrika Kusini, Rwanda na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo katika tamasha hilo la nyimbo za injili za kumsifu Mungu.

0 maoni: