KANISA la Christian Mission Fellowship la Sinza jijini Dar es Salaam, limetoa msaada wa baiskeli 100 kwa watu wenye ulemavu nchini zilizogharimu sh. Milioni 52.
Baiskeli hizo zimegawanywa katika mikoa mitatu, ambapo Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, imepata baiskeli 50, Mkoa wa Mpanda 30 pamoja na Tunduru Kusini 20.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, jana wakati wa makabidhiano ya baiskeli hizo Askofu wa kanisa hilo, Dk Mgullu Kilimba alichanganua kuwa baiskeli hizo zimetolewa na wafadhili kutoka Marekani.
Akipokea msaada wa baiskeli hizo kwa niaba ya wizara hiyo, Naibu waziri, Philipo Mulugo alisema baiskeli hizo zimekuja kwa wakati muafaka ambapo serikali ipo katika mchakato wa Sensa itakayobaini idadi ya walemavu wanaohitaji msaada huo.
Mulugo alifafanua kuwa serikali itashirikiana na taasisi za dini katika kutatua changamoto zinazowakabili walemavu wa aina mbalimbali nchini.
“Baiskeli hizi zitakuwa chachu kwa walemavu wetu kwa sababu zitawawezesha kufanya shughuli mbalimbali za maendeleo tofauti na awali, hata hivyo serikali itashirikiana na taasisi hizo kwa sababu wafadhili wengi wanapitia huko kwa gharama nafuu” kwa mujibu Mulugo.
Katika hilo alikiri serikali kutokuwa na uwezo wa kugharamia vifaa vya walemavu kutokana na kuuzwa ghali, jambo ambalo limewasababishia wengi wao kuendelea kuishi katika mazingira hatarishi au kutojihusisha na shughuli za maendeleo.
Naye Mbunge wa Mpanda vijijini Moshi Kakoso (CCM), alisema baiskeli hizo zitawasaidia wananchi wa jimbo hilo hususan wenye huitaji maalumu.
Kwa upande wa Mbunge wa Tunduru Kusini(CCM), Mtura Abdallah alizitaka taasisi nyingine kuiga mfano wa kanisa hilo, ili kuwawezesha walemavu kupata fursa ya kufanya shughuli mbalimbali za maendeleo katika jamii.









