Wanachama wa Kituo wamefanya kikao cha kazi pamoja na Mfuko wa LAPF leo, Agosti 25, 2012, kwenye Hoteli ya Nashera iliyopo mjini Morogoro. Lengo la kikao hicho, ambacho kilihusisha wanachama 25 wa Kituo na wataalamu wa LAPF, ilikuwa ni kuwawezesha washiriki kuelewa kazi za mfuko ili waweze kuhariri vema zaidi habari mbali mbali, hususan zile zinazohusu masuala ya mfuko huo.
Akifungua kikao hicho, Meneja Masoko na Uhusiano wa Mfuko huo, Bw. Andrew Kuyeyana, alisisitiza umuhimu wa kutoa mafao bora zaidi kwa wanachama ili kuwawezesha kustaafu vema. Alisema Mfuko wake, ambao hadi kufikia Juni mwaka huu ulikuwa na zaidi ya wanachama 90,000, unafanya juhudi kufanikisha hilo kupitia mafao mbali mbali, ikiwa ni pamoja na pensheni, mafao kwa warithi, uzazi, gharama za mazishi, mikopo ya ujenzi wa nyumba na mikopo kwa Saccos.
Akiwasilisha mada kuhusu shughuli za Mfuko wa LAPF, Meneja za Mfuko huo kwa Kanda ya Mashariki, Bw. Sayi Lulyalya, alisema miongoni mwa mipango ya baadae ya Mfuko ni kuanzisha mafao ya elimu ili kuwapa faida zaidi wanachama.
Naye Meneja wa Mipango na Uwekezaji wa Mfuko huo, Bw. Elias Baruti, alisema miongoni mwa changamoto zinazoukabili Mfuko ni jinsi ya kuwezesha upatikanaji wa faida ya kuridhisha katika hali ya uchumi ambao unaathiriwa na mfumuko wa bei.
Meneja huyo alisema miongoni mwa mipango ya baadaye ya Mfuko huo ni kuwezesha ujenzi wa miji midogo (satellite towns) katika maeneo mbali mbali nchini ili kutoa nafasi za ofisi na biashara.
Akitoa neno la shukrani, Mwenyekiti wa Kituo, Lauden Mwambona, alisema wahariri wasanifu na watayarishaji vipindi wanatakiwa kuwa na uelewa mkubwa na wa kina zaidi wa masuala mbali mbali ya kitaifa na kimataifa ili waweze kuhariri habari kwa ufanisi zaidi.




