Majambazi wanne wameuwawa mkoani Tabora wakati wa mapambano makali ya kurushiana risasi baina yao na Askari Polisi baada ya jaribio lao la kutaka kuvamia eneo la Congres centre kuzuiwa na jeshi hilo huku wakiwa wamejifunika usoni kwa vitambaa.
Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tabora, Kamishna Msaidizi wa Polisi Antony Rutta alisema tukio hilo lilitokea Agosti 25 mwaka huu majira ya saa tisa mchana katika kijiji cha Kaliua Magharibi, wilayani Kaliua Mkoani Tabora.
Kamanda Rutta alisema eneo hilo ambalo lilitaka kuvamiwa na majambazi la Congres Centre ni eneo ambalo hutumiwa na wafanyabiashara wengi kufanya biashara zao.
Alisema majambazi hao walikuwa wakitumia Bunduki aina ya Shot gun ambapo baada ya tukio hilo bunduki hiyo ilipatikana ikiwa na risasi 12 na maganda sita ya risasi za Shot gun yaliokotwa eneo la tukio.
Aidha baada ya kutolewa vitambaa usoni jambazi mmoja aliyeuwawa ametambulika kwa jina la Masud Haruna mkazi wa Kijiji cha Imalamihayo, wilayani Kaliua na wengine watatu bado hawajatambulika.
Katika hatua nyingine Jeshi la Polisi Mkoani Tabora limetoa wito kwa wananchi kuendelea kutoa taarifa za uhalifu na wahalifu kwa Jeshi hilo ili kuhakikisha wale wote wanaojihusisha na vitendo hivyo wanakamatwa na kufikishwa kwenye vyombo vya sheria.





