Hatimaye zoezi la kuwahesabu Wahadzabe waishio wilayani Karatu lafanikiwa kwa asilimia mia moja baada ya wanajamii kujitokeza kwa wingi kuhesabiwa ambapo wameitaka serikali kutimiza ahadi zao wakati wa uhamisishaji ili kuona matokeo ya zoezi hilo.
Walionyesha furaha yao wakati wa kuhesabiwa baada ya kukabidhiwa nyama ya punda milia 15 kama ushawishi wa kujitokeza kuhesabiwa walisema kuwa wanaishukuru serikali yao hasa ya awamu hii kwa kuwakumbuka na kuona umuhimu wa wao kuhesabiwa.
Akiongea kwa niaba ya wenzake Martha Daniel alisema kuwa wao kama wao ni jamii ambayo mara nyingi wamekuwa wakiishi porini na kutegemea matunda na wanyama wa porini ambapo kwa sasa wamevamiwa na makabila wengine na kuchunga mifugo yao na kukata miti katika makazi yao hali iliyosababisha maisha yao kuwa magumu zaidi.
Aliongeza kuwa kutokana na kuvamiwa na makabila hayo wamekuwa wakikosa chakula hali ambayo wamekuwa wakiishi mazingira ya shida sana hivyo wameiomba serikali kuwaamisha makabila mengine katika pori hilo wanaloishi au kuwatafutia eneo lingine watakalofanikiwa kupata matunda na wanyama pori ilivyokuwa mwanzo.
Naye Shako Sigwazi aliiomba serikali kutimiza yale waliyowaahidi wakati wa kuwaelimisha kuhusu swala sensa kwani wamekuwa ni watu wanaoishi porini kama wanyama hali inayowafanya kujiona kama wamesahaulika na serikali yao.
Pia aliongeza kuwa wao kama wao wameshachukia mazingira hayo na kuiomba serikali na wananchi wote kuondokana na imani kuwa wao hawataki kurekebishiwa mazingira ya kuishi kama binadamu wengine wanaoishi wakiwa na huduma zote za kijamii.
Akifafanua zaidi uboreshwaji wa mazingira alisema kuwa wanahitaji kuwa huduma zote za kijamii ikiwemo na miundombinu ya maji, afya barabara umeme, n.k ili nao waweze kujivunia kuwa ni Watanzania wanaothaminiwa na serikali yao.
Kwa upande wake mkuu wa Wilaya hiyo ya Karatu Daudi Felex Mtibenda aliwashukuru wananchi hao wa jamii ya kihadzabe kwa kujitokeza na kuunga mkono zaozi hilo la kukubali kuhesabiwa na hii ni baada ya jamii hiyo kukataa kuhesabiwa na kutoa masharti ya kuletewa kwanza bangi, pombe haramu aina ya gongo na nyama ya nyani kwa madai kuwa wao hawaoni maana yoyote ya wao kuhesabiwa.
“Kwanza niwapongeze ndugu zangu kwa kuniunga mkono kwa kujitokeza kwa wingi kuhesabiwa hivyo kwa kuwa tumepata idadi yenu na mahitaji yenu, serikali itakuwa pamoja nanyi katika kuhakikisha maendeleo yanakuwepo kwa jamii nzima wakiwemo nanyi wahadzabe” alisema Mtibenda.
Baada ya kukabidhi nyama hiyo ya pundamilia 15 kwa jamii ya wahadzabe pia alitembelea machimbo ya madini ya dhahabu ya Murus yaliyoko kata ya Endabash na kufanikiwa kuongea na wachimba madini kuwahamasisha katika kushiriki katika zoezi hilo.
Kwa upande wa wafanyakazi wa machimbo hayo ya dhahabu ya Murus walisema kuwa wako tayari kuhesabiwa na kuiomba serikali kuwaboreshea miundo mbinu katika maeneo hayo ikiwemo huduma za kijamii hasa haspitali.
Awali wakati wa kuhesabiwa usiku wa Agost 25 kuamika 26 mkuu huyo aliwakusanya watoto wanaoishi katika mazingira magumu (mtaani)wapatao 26 na kuwahamasisha kuhesabiwa ili kupatiwa mazingira mazuri ya kuishi kwa kujengewa kituo chao na kupatiwa huduma muhimu ikiwemo mavazi na malazi.
Naye mmoja wa watoto hao mwenye malengo ya kuwa Rais aliyejitambulisha kwa jina laEdson Julius (12) aliiomba serikali kuwasaidia kuwapatia huduma hizo pamoja na elimu ili kufanikiwa kutimiza malengo yao kwani wamechoka maisha ya kuishi mitaani na kulala mitaroni pamoja na kuitwa machokoraa.





