Marehemu Kardinal Laurean Rugambwa enzi ya uhai wake.
Kanisa kuu katoliki jimbo la Bukoba ambalo masalia ya marehemu kardinali Rugambwa yatazikwa ndani yake.
Kanisa katoliki nchini dayosisi ya Bukoba mkoani Kagera, wanajiandaa kuzika upya masalia ya mwili wa aliyekuwa askofu wa dayosisi hiyo Kardinali Laurean Rugambwa, aliyefariki mnamo mwaka 1997 katika kanisa kuu la Bukoba. Maziko ya Kadinali Rugambwa yamepangwa kufanyika siku ya oktoba 6 mwaka huu.
Mwili wa askofu huyo wa kwanza nchini na Kardinali wa kwanza mweusi barani Afrika umezikwa katika kanisa la kwanza mkoani Kagera lililopo Kashozi kutokana na kwamba kanisa kuu la Bukoba ambalo marehemu aliagiza kuzikiwa ndani yake lilikuwa katika matengenezo makubwa.
Akizungumza katika kipindi cha Baragumu Channel ten na baadaye kwenye mkutano na waandishi wa habari jijini Dar es salaam, Askofu msaidizi wa Jimbo la Bukoba Askofu Methodius Kilaini , amesema wanataka kumzika kardinali Rugambwa kwa heshima tena katika kanisa alilopenda kuzikiwa kutokana na kukamilika kwake, lakini kabla ya kuzikwa humo kutatanguliwa na ibada mbalimbali ikiwa sehemu alikozaliwa, alikobatizwa, sherehe zitakazoambatana na kusherehekea miaka 100 ya kuzaliwa kwa kardinali Rugambwa tarehe 7 mwezi Octoba.








