MBUNGE wa Viti maalum wa Mkoa wa Tanga Amina Mwidau (CUF)
………………………………………
Na Mwandishi Wetu, Pangani
MBUNGE wa Viti maalum wa Mkoa wa Tanga Amina Mwidau (CUF), amekabidhi mifuko ishirini ya Saruji kwa ajili ya kuunga mkono juhudi za Serikali ya Kijiji cha Kipumbwi katika ujenzi wa shule ya Msingi .
Akihutubia mkutano wa hadhara uliofanyika jana kijiji hapo Mwidau, alisema kuwa ili kuweza kujenga jamii imara ni lazima kuhakikisha elimu inapewa kipaumbele cha pekee.
“Sina budi kuunga mkono juhudi zenu za ujenzi wa shule ya Kipumbwi Mtoni, ambayo imejengwa kwa nguvu za wananchi nami kama mwakilishi wetu ninangana nanyi kwa dhati na katika hili ninapenda kukabidhi mifuko hiyo ya saruji.
“Kwa kipindi cha siku kadhaa nimekuwa na ziara katika mkoa wa Tanga lakini nilipofika katika kijiji cha Mkwaja hali ni mbaya sana shule yenye wanafunzi zaidi ya 300 lakini ina waalimu wanne tu.
“Mbali na hali hiyo kati ya watoto hao watoto 283 wa darasa la kwanza hadi la Saba hawajui kusoma wala kuandika je hapa wa kulaumiwa ni nani. CCM imeshindwa kusimamia sera ya elimu kwa vitendo na sasa hawana budi kuadhibiwa nanyi wananchi kutokana na hali hii.
“…, serikali imekuwa haina mpango katika kuinua elimu kwani imekurupuka katika ujenzi wa shule za Sekondari za Kata hali ya kuwa haina mpango wa kuajiri waalimu wengi zaidi.
Na hata waalimu waliopo kila kukicha ni matatizo na Serikali ambayo kwa muda mrefu iliahidi kulipa madai yao lakini hadi leo wameshindwa hali inayopelekea waalimu kuaadhibu watoto kwa kutowapa elimu bora darasani,” alisema Mwidau
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kijiji cha Kipumbwi Jamali Nassoro, alimshukuru mbunge huyo kwa kuunga mkono juhusi za wananchi katika kunua sekta ya elimu wilayani Pangani.









