MPANGO WA UGAWAJI WA PEMBEJEO WABADILIKA ,WAKULIMA SASA KUPATA MBEGU NA MBOLEA KWA WAKATI

Na Gladness Mushi wa Fullshangwe-Arusha

Imeelezwa kuwa kutokana na hali ya udanganyifu wa pembejeo za kilimo ambazo zilikuwa zinasambazwa chini ya mawakala na makampuni mbalimbali kumesababisha madhara makubwa sana kwa wakulima huku hali hiyo ikisababisha hata uhaba wa chakula

 Kauli hiyo imetolewa na Mkuu wa mkoa wa Kilimanjaro Bw. Leonidas Gama wakati akifungua mkutano kwa maafisa kilimo wa mkoa wa Kilimanjaro,Arusha,Manyara na Singida mapema leo mjini Arusha

 Alisema kuwa kwa sasa hali hiyo itabadilishwa kutokana na Serikali kubadilisha hata aina ya utoaji wa pembejeo kwani mpango mkakati ambao ulikuwa ukitumika hapo awali ulikuwa ni chanzo pekee cha kuweza kuwakwamisha hata wakulima hasa ngazi za Vijijini

 Bw. Gama alifafanua kuwa mpango huo ambao utaanza kwa msimu ujao wa kilimo utakuwa ni mpango wa kukopeshana kupitia katika vyama vya kuweka na kukopa(SACCOS),vyama vya Ushirika huku mpango huo ukiweza kuwasaidia wakulima wa vijijini

 Alibainisha kuwa kupitia mfumo huo mawakala na kampuni zao ambazo hazina uwezo wa kuwasaidia wakulima hazitaweza kufanya kazi hiyo kwani mfumo huo pia utafanya mabadiliko makubwa kwani watakaohusika na kusambaza pembejeo ni Makampuni

 “Makampuni ambayo yatahusika na hii kazi ndiyo yatakayotambua aina ya mawakala ambao wanaofanya nao kazi na kama wakiwa wabaya sisi tutawashika makampuni nah ii itachangia kwa kiwango kikubwa sana kupunguza hata changamoto mbalimbali ambazo zilikuwa zinawakabili wakulima na kwa sasa tuna uhakika hata wa kuongeza kiwango kikubwa sana cha chhakula kuanzia ngazi ya kaya”aliongeza bw Gama

 Awali alisema kuwa ili mpangoi huo uweze kufanikiwa ni lazima wizara kwa kushirikiana na wadau wengine watoe elimu kwa wakulima, vyama vya ushirika, na saccos juu ya mabadiliko hayo, ambapo endapo serikali itashindwa kuwapa elimu huenda zoezi hilo likakwama kutokana na vyama hivyo kushindwa kurejesha mikopo kwa wakati. .

Naye Mkurugenzi msaidizi wa pembejeo za kilimo kutoka wizara ya kilimo chakula na ushirika,Dkt Mshindo Msolla alisema kuwa,vikundi na vyama vya ushirika ni lazima viandaliwe na vikaguliwe na kuwa na mikataba ya kuuzia bidhaa zao pindi watakapozalisha.

Alisema kuwa, kupitia mfumo huo , itawezesha kwa kiasi kikubwa sana kuweza kuondokana na mawakala wasio waadilifu ,ikiwa na ni pamoja na makampuni yenye pembejeo feki kutochaguliwa tena na hivyo kuwezesha kuwapatia wakulima pembejeo zenye ubora na kwa wakati muafaka.

Aliongeza kuwa, kupitia mfumo huo mawakala wa pembejeo watateuliwa na makampuni ya pembejeo   ambapo wakala mmoja ana uwezo wa kuwakilisha zaidi ya kampuni moja na wakala zaidi ya mmoja kufanya kazi kwenye kijiji ili kuongeza ushindani.

MIMI NI MPIGA PICHA NA MWANDISHI WA HABARI WA KUJITEGEMEA NA KUPITIA BLOG HII NINA IMANI TUTAWEZA KUPEANA HABARI MBALIMBALI ZA BURUDANI ZITAKAZOFURAHISHA NA KUELIMISHA NAOMBA USHIRIKIANO WENU ILI TUWEZE KUFIKA TULIPOKUSUDIA

Got something to say? Go for it!