Na Gladness Mushi wa Fullshangwe- Arusha.
MKAZI mmoja wa Unga ltd jijini Arusha aliyefahamika kwa jina la Mudy Mussa (27) amefariki dunia baada ya kushambuliwa na wananchi wenye hasira kali wakati akijaribu kupora yeye na wenzake .
Kamanda wa polisi mkoani hapa, Liberatus Sabas alisema kuwa tukio hilo limetokea septemba 16 mwaka huu majira ya saa 5;30 usiku katika kata ya Pori wilayani Arumeru mkoani Arusha.
Alisema kuwa, tukio hilo lilitokea baada ya marehemu pamoja na wenzake ambao bado hawajafahamika kuvunja uzio wa jengo la Tumaini Farm kwa nia ya kuiba ndipo walinzi wa eneo hilo walipopiga kelele za kuomba msaada kwa majirani hali iliyosababisha wananchi kuamka na kufanikiwa kumkamata mtuhumiwa huyo ambapo walimshambulia na kumsababishia majeraha makubwa sehemu za mwili wake.
Aidha Kamanda Sabas alifafanua kuwa, baada ya tukio hilo polisi walimchukua na kumpeleka katika hospitali ya mkoa ya Mount Meru kwa ajili ya matibabu lakini alifariki dunia akiwa njiani.
Aidha mwili wa marehemu umehifadhiwa katika chumba cha kuhifadhia maiti cha hospitali ya Mount Meru kwa ajili ya uchunguzi wa daktari na jeshi la polisi mkoani hapa linaendelea kuwatafuta wale wote waliohusika katika kujichukulia sheria mkononi na kusababisha mauaji hayo .
Alisema kuwa, polisi pia inaendelea na uchunguzi zaidi wa kuwasaka wale wote waliokuwa wakishiriki katika uhalifu huo kwa nia ya kuiba ,hivyo aliwaomba wananchi mbalimbali kuhiriki kikamilifu katika kuwafichua wahalifu .








